Benki ya CRDB Kutoa gawio kwa Wanahisa la TZS bn 19 kwa mwaka 2011-2012

Benki ya CRDB inatarajia kutoa gawio la shilingi bilioni 19 kwa wanahisa wake  kwa kipindi cha mwaka 2011- 2012 kama sehemu ya faida ya shilingi bilioni 37 ambazo benki imepata kwa kipindi hicho.

Mkurugenzi mtendaji wa benki ya CRDB Dkt Charles Kimei alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha alipokuwa akitoa taarifa za awali kuhusu mkutano mkuu wa 17 wa wanahisa tangu kubinafsishwa toka mikononi mwa serikali mwaka 1996.


Dkt Kimei aliongeza kuwa mkutano huo pia utafanya uchaguzi wa wakurugenzi watatu wapya, wakurugenzi mbao wanapaswa kuchaguliwa na wanahisa hao baada ya wale wa zamani kumaliza muda wao.


Dkt Kimei alisema mkutano huo utafanyika kwa mujibu wa sheria ya makampuni sehemu ya 133 na kwamba mkutano huu ni muhimu sana ambao wanahisa wote wanatakiwa kuhudhuria ili kujua jinsi hisa zinavyotunzwa .

Aliongeza kuwa pamoja na masuala mengine wanahisa watapewa taarifa ya mahesabu ya biashara ya mwaka uliopita unaoishia 2011 na kuwapa taarifa za maendeleo ya benki.

Dkt Kimei alifafanua kuwa benki hiyo inakila sababu ya kutoa sehemu ya faida kwawanahisa wake kwakuwa mtaji wa benki hiyo umepanda na CRDB ndiyo benki yenye mtaji mkubwa kuliko benki nyingine  hapa nchini.

Aidha aliwataka Watanzania kutambua umuhimu wa kuwa na hisa kwani wengi wameonekana kukosa mwamko na nafasi yao kuchukuliwa na watu wa nje baada ya watanzania kuonekana kuwa hawatambui umuhimu wa kumiliki hisa.

“Watu wengi wamekuwa wakiuza hisa mtaani kwa bei ya hasara jambo ambalo linasababisha kushuka kwa thamani za hisa na kutofikia malengo waliojiwekea wakati wakinunua hisa” alisema Dkt Kimei.

Aliongeza kuwa mkutano huo utafuatiwa na semina  kwa waandishi wa habari ambayo itafanyika jijini Dar-es-salaam yenye lengo la kuwapa ufahamu wanatahaluma hao ili kutambua kazi za benki hiyo na namna inavyotoa huduma kwa wateja wake wanaoiwezesha benki kufikisha mtaji wa zaidi ya shilingi bilioni 250 hadi sasa.